Mifugo 5,219 yahamishiwa Msomera

0
138

Mifugo 5,219 ya wafugaji wanaoishi eneo la hifadhi ya Ngorongoro, hadi kufikia leo Septemba Mosi imehamishiwa katika kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga tangu kuanza kwa zoezi la kuwahamisha wananchi walio tayari kuhama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro.

Taarifa hiyo imetolewa leo wakati wa kuaga kundi la 7 la kaya 25 zenye watu 159 walioondoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomera kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella ameeleza kuwa tangu kuanza kwa zoezi la kuhamisha wakazi walio tayari kuhamia Msomera Juni 26 mwaka huu hadi kufikia Septemba Mosi mwaka huu, jumla ya kaya 158 zenye watu 794 na mifugo 5,219 zimeandikishwa na kuhamishiwa katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga.

“Zoezi hili tulianza tarehe 16 Juni, 2022, hamasa imekuwa kubwa kuliko tulivyotarajia, katika awamu zote leo kundi hili la 7 ndio lina kundi kubwa la mifugo ipatayo 2,109. Hii ni ishara njema katika kupunguza muingiliano wa wanyamapori na mifugo ndani ya hifadhi.” ameongeza Mongella.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt. Christopher Timbuka amebainisha kuwa idadi ya wananchi wanaojitokeza kujiandikisha na kuhama kwa hiari imeendelea kuongezeka kutokana na hamasa na elimu iliyotolewa kwa wananchi hasa baada ya serikali kujenga miundombinu ya huduma za kijamii kama shule, hospitali, huduma ya maji, majosho, Malambo, barabara, nyumba za kuishi, mashamba, nishati ya umeme pamoja na mawasiliano.

Dkt. Timbuka ameongeza kuwa zoezi la kuhamisha wananchi hao linazingatia misingi na taratibu zote za haki za binadamu pamoja na muongozo wa uhamishaji wa wakazi ulioandaliwa na Serikali.

Saruni Mapekuo kutoka kijiji cha Kapenjiro ambaye ni mmoja wa wananchi wanaohama kwa hiari ameeleza kuwa;

“Tunashukuru kwa fursa hii tuliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutupa fursa ya kuhama Ngorongoro kwenda Msomera.

Zoezi la uhamasishaji na uandikishaji wa Wananchi kuhama kwa hiari linaendelea, ambapo hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2022 jumla ya kaya 1,019 zenye jumla ya watu 5,667 na mifugo 13,927 zimejiandikisha kuhama kwa hiari katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro.