Shirikisho la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) limeweka hadharani mpango mkakati wa kutumia njia ya michezo kuhamasisha amani duniani badala ya kutumia njia ya vita.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Ngome, jijini Dar es Salaam, Balozi wa CISM, Kanali Dorah Mamby Koita raia wa nchi ya Guinea, ambaye kwa sasa ni Mwambata Jeshi wa nchi ya Guinea nchini Ubelgiji ameviambia vyombo vya habari kuwa ipo haja ya Nchi za Afrika kufahamu kikamilifu jinsi ya kutumia michezo ili kujijengea nguvuĀ za kisiasa na ushawishi duniani.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa michezo
unapovuka nje ya mipaka ya kitaifa inajenga urafiki wa karibu wa kidiplomasia ambapo michezo ni kipengele muhimu zaidi kutekeleza diplomasia nchini.
Hata hivyo Kanali Dorah ameongeza kuwa michezo inaweza kutumika kama chombo cha kuchochea maelewano wakati mahusiano kati ya mataifa mawili ni duni na ikiwa mahusiano yatatengamaa, michezo pia inaweza kuunda na kuharakisha kasi ya kidiplomasia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani, Kanali Joseph Bakari amesema moja ya mikakati ya baraza hilo nikutumia nchi zilizokuwa zikikutana katika uwanja wa vita sasa kukutana katika viwanja vya michezo ili kuhamashisha amani.
Ameongeza kusema mikakati mingine ni kuhamasisha michezo kuchukuliwa kama fani kwenye nchi za Afrika na maandalizi yake kuwa endelevu na yenye kulenga kufanya vizuri.
Akitoa mifano ya nchi zinazofanya vizuri amesema linapokuja suala la ushiriki wa mashindano ya michezo kwa upande wa nchi nyingine wao huanza maandalizi ya mashindano hayo miaka saba kabla.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Duniani, Brigedia Selemani Gwaya amesema shirikisho hilo kwa sasa halifahamiki kama inavuotegemewa kwa sababu ushiriki katika michezo ni mdogo hivyo sasa inabidi kuweka jitihada zaidi katika kulitangaza shirikisho hilo.
Shirikisho la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM ) lina wanachama 140 ambapo nchi za Afrika ni 47, Amerika 19, Asia 32 na Ulaya 42. Hadi sasa shirikisho hilo limefikisha miaka 74 toka kuanzishwa kwake mwaka 1948.