Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi imewahukumu washtakiwa wanne wa kesi ya madawa ya kulevya aina ya bangi akiwemo raia wa nchini Poland na mwengine mwenye asili ya Kieshia miaka 30 jela, kulipa faini pamoja kutaifisha mali walizokutwa nazo washtakiwa hao.
Akitoa hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba CC 79/2020, Hakimu Mwandamizi mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi Bernadeta Maziku amesema mshtakiwa namba moja Damian Krzysztof pamoja na Mshitakiwa namba mbili ambaye ni mke wa mshtakiwa namba moja , Eliwaza Pyuza wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa makosa mawili ikiwemo kosa la ustawishaji wa mimea iliyokatazwa pamoja na kusafirisha dawa za kulevya.
Hakimu huyo ametoa hukumu kwa mshtakiwa namba mbili Eliwaza Pyuza, mshitakiwa namba 3 mwenye asili ya kieshia Hanif Kanan na mshitakiwa namba 4 Boniface Kessy kifungo cha miaka 3 au kulipa faini ya shilingi milioni 4 kila mmoja kwa kosa la kutumia madawa ya kulevya kinyume cha sheria namba 18 ya mwaka 2015 iliyofanyiwa marejeo ya sheria namba 5 ya mwaka 2017.
Nje ya mahakama hiyo, Kaimu Kamishna wa kitengo cha Huduma za Sheria Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Christina Gervas pamoja na wakili wa upande wa serikali Ignas Mwinuka wameridhika na hukumu hiyo ambayo itatoa fundisho katika jamii.
Hata hivyo Mahakama ya Hakimu mkazi mjini Moshi imeagiza kutaifishwa kwa mali zote zilizokutwa na washtakiwa hao ikiwemo shamba, majaba yaliyokuwa yakihifadhia bangi pamoja na pesa taslimu zaidi ya shilingi milioni 26.