Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli ameahidi kulinda tunu za Taifa zilizoachwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwa ni kuenzi tangu alipofariki miaka 21 iliyopita.
Dkt. Magufuli amesema hayo wakati wa kampeni katika Uwanja vya Tanganyika Packers akiomba ridhaa ya wana-CCM na wananchi kumchagua kuwa Rais kwa awamu ya pili na kuchagua wabunge na madiwani wa CCM kwa miaka mitano ijayo.
Tunu hizo ni Pamoja na uhuru wa Taifa la Tanzania, amani na utulivu, umoja na mshikamano, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ujenzi wa Taifa la kujitegemea lenyewe kwa kutumia rasilimali zake.
“Kwa kutumia hiyo misingi mitano serikali ya awamu ya tano katika miaka mitano iliyopita imejitahidi kuyatekeleza maono ya Baba wa Taifa. Nitakapochaguliwa kuongoza Tanzania nitahakikisha tunu hizi nazilinda kwa nguvu zetu na hasa muungano wetu.”
Katika hatua nyingine mgombea huyo wa urais amesema wananchi wa Jimbo la Kawe wakimchagua mgombea ubunge wa jimbo hilo, Askofu Josephat Gwajima, serikali yake itatenga fedha kwa ajili ya kijenga bandari ya katika Jimbo hilo.
Dkt. Magufuli amehitimisha kampeni katika Jiji la Dar es Salaam ambapo anatarajia kuendelea na kampeni mkoa mingine.