Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa kipindi cha miongo kadhaa mfumo wa haki jinai nchini umevurugika kutokana na kupuuzwa kwa mifumo ya maadili iliyopo katika kila taasisi.
Dkt. Samia ameyasema hayo Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma alipokuwa akizindua tume ya kuangalia namna ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini.
Amesema hatua ya kupuuza mifumo ya maadili katika taasisi imesababisha kupotea kwa haki za watu wasio na uwezo wakimamlaka au fedha na wengine wasio na makosa kubambikiwa makosa huku wakosaji wakiepushwa na makosa kutokana na uwezo wao kifedha.
Rais Samia amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuipitia upya mifumo ya taasisi, ili kubaini wapi kuna makosa na namna ya kuboresha kasoro au makosa hayo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, miongoni mwa watu aliowateua kuwa wajumbe wa tume hiyo yenye lengo la kuangalia namna ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini wametoka kwenye taasisi hizo zinazokwenda kuchunguzwa akizitolea mfano kuwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), Ofisi ya Taifa ya mashtaka, Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, Jeshi la Magereza, Jeshi la polisi na Mahakama.