Meli kubwa ya watalii yawasili nchini

0
177

Bandari ya Dar es Salaam, leo imepokea meli ya watalii iliyobeba watalii 1,060 pamoja na wafanyakazi 587 wa meli hiyo ambao watafanya utalii katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam na maeneo jirani kabla ya meli hiyo kuendelea na safari yake.

Tayari watalii hao wameanza kufanya utalii katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam, Bagamoyo mkoani Pwani na katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mathew Anthony amesema, bandari hiyo imekuwa ikipokea meli zenye ukubwa huo hasa mara moja kwa mwaka na kwamba wanaandaa mikakati ya kufanya biashara baina ya watanzania na watalii wanaotumia bandari hiyo

“Sasa hivi tumeishaamua tutajenga gati la meli za watalii ambalo litakuwa na malls [maduka makubwa] nyingi ndani, wataingia ndani ya nchi yetu, wataingia ndani ya hizo malls [maduka makubwa] watatuachia dola za kutosha ndani ya nchi yetu.” amesema Anthony

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Amos Nnko amesema, kuwasili nchini kwa meli hiyo ya watalii ni hatua muhimu katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo na amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kukuza utalii nchini.

Meli hiyo ya Zaandam ilianza safari yake nchini Marekani Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na watalii kutoka mataifa mbalimbali na itakaa Tanzania Bara kwa muda wa siku mbili na kuelekea Zanzibar ambapo pia itakaa kwa muda wa siku mbili na itamaliza safari yake Desemba 10 mwaka huu.

Meli hiyo ya watalii yenye urefu wa futi 781 na upana wa futi 105.8 ina uwezo wa kubeba watu 1,432 na ni meli ya watalii ya kwanza kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam baada ya janga la UVIKO -19.