Mdee ataka wabunge wapimwe corona

0
310

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) ametaka wabunge wote wapimwe kama wana maambukizi ya virusi vya corona ama la, na watakaobainika kuwa na maambukizi wapelekwe karantini.

Mdee ameyasema hayo leo bungeni wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai alipomaliza kueleza mabadiliko ambayo bunge imechukua ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo kwa watu wote watakaokuwa kwenye viwanja wa bunge wakati wote.

“Mheshimiwa Spika, kwanini tusianze na sisi tupimwe wote [tupimwe corona] tukijijua tupo salama tukae hapa tu ‘debate’ (tujadiliane)? Hili ndio bunge la mwisho mheshimiwa kuelekea uchaguzi mkuu,” amesema Mdee.

Akijibu hoja hiyo Spika Ndugai amesema kuwa wazo hilo ni zuri na kwamba mamlaka husika imelichukua na itaona namna ya kulifanyia kazi.

Akieleza mabadiliko ambayo bunge imechukua kudhibiti virusi vya corona, Ndugai amesema kuwa bungeni wataingia wabunge 150 tu, hakutakuwa na maswali na majibu kwa waziri mkuu, maswali kwa wizara yatatumwa kupitia ‘tablets’ na majibu yatatolewa kwa njia hiyo hiyo.

Bunge hilo la bajeti limeanza leo mjini Dodoma na litafanyika kwa saa nne, kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 jioni.