Kufuatia kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Machi 19, 2021, nafasi ya Makamu wa Rais imebaki tupu.
Rais Samia alikuwa akishikilia nafasi hiyo ya Makamu wa Rais tangu mwaka 2015 hadi kuapishwa kwake.
Je, mchakato wa kumpata Makamu wa Rais upoje?
Kifungu cha 37(5) kinamtaka Rais baada ya kuapishwa kukaa na wanachama wa chama chake ambacho kwa sasa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuchagua mtu wa kushika wadhifa huo.
Na kisha Rais kuwasilisha jina hilo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya Wabunge kupiga kura.
Hii leo Dkt. Philip Mpango amependekezwa kuwa Makamu wa Rais. Ili kushika wadhifa huo, lazima kura atakazopigiwa zifikie akidi (zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa ziwe kura za ndio).
Akishinda, Dkt. Mpango atatakiwa kuapishwa kama isemavyo Ibara ya 49 na 50(4)
“Makamu wa Rais, kabla ya kushika madaraka yake ataapishwa mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge,” Ibara ya 49.
“Ikitokea kwamba kiti cha Makamu wa Rais ki wazi kutokana na masharti yaliyomo katika ibara ya 50(3), kifo au kujiuzulu basi mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote ndani ya siku zisizozidi kumi na nne baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura za Wabunge walio wengi,” Ibara ya 50(4)
Samia Suluhu Hassan ameachia kiti hicho na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli.