Mbunge wa Nachingwea akabidhi vifaa vya milioni 22 kiboresha elimu

0
213

Mbunge wa Jimbo la Nachingwea mkoani Lindi, Amandus Chinguile amekabidhi mifuko ya saruji 1,800 ikiwa ni moja ya ahadi zake katika sekta ya elimu aizotoa wakati akiomba ridhaa katika uchaguzi Mkuu 2020.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa katika kata 16 kwa lengo la kuboresha miundombinu ya shule za sekondari ndani ya kata hizo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Chinguile amesema yeye kama mbunge anao wajibu wa kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira rafiki kwa kuwaboreshea miundombinu.

Amesema kuwa ataendelea kuziangazia shule zenye changamoto na kuziwekea mazingira rafiki ya kujifunzia.

“Ni wajibu wetu sisi kama viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha tunashirikiana kwa pamoja kuinua elimu katika wilaya yetu kwa kuhakikisha tunaiboresha miundombinu ya shule,” amesema Chinguile.

Vifaa hivyo vinatarajia kutumika kakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 22 katika shule za sekondari zilizopo Jimboni humo.