Mbunge atoa ushuhuda alivyougua na kupona corona

0
522

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia amekiri kuwa ni kweli alipata maambukizi ya virusi vya corona, na kwamba sasa amepona na amerejea bungeni kuendelea na shughuli zake.

Akizungumza wakati wa kikao cha bunge mjini Dodoma amesema kwamba alikuwa mtu wa pili kufika katika kituo kilichotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wenye maambukizi, na ameishukuru serikali kwa huduma bora alizopatiwa pamoja na wenzake.

“Nimerudi kwenye bunge lako tukufu kukwambia kuwa nimepona. Nimekaa kituo cha Mkonze Dodoma, kuanzia tarehe 19 mwezi Aprili, mpaka tarehe 13 mwezi Mei, kwa muda wote huo hakijawahi kutokea kifo hata kimoja,” amesema Mtulia.

Aidha, amewataka Watanzania kutokuwa na hofu, na kuongeza kwamba ni kweli virusi vya corona vipo lakini vinatibika.

“Naungana na Mhe. Rais kwamba, ugonjwa upo, tahadhari tuchukue, lakini tusijenge hofu kubwa,” amesisistiza kiongozi huyo.