Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema lengo la serikali ni kuufanya mkoa wa Mbeya kuwa kitovu cha biashara kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami kutoka Nsalaga hadi uwanja wa ndege wa Songwe.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika licha ya kupunguza foleni katikati ya jiji la Mbeya, pia utarahisisha shughuli za uzalishaji kwa mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe.
Aidha, Profesa Mbarawa amesema, mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami kutoka Nsalaga hadi uwanja wa ndege wa Songwe utaongeza chachu ya maendeleo na kuunganisha wafanyabiashara kutoka nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaoagiza bidhaa zao kutoka nje kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Mradi huo ni wa miaka miwili na utatumia shilingi bilioni 138, ambazo ni fedha za serikali kwa asilimia mia moja.