Majaliwa: Imarisheni uhifadhi wa mazingira

0
146

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amehimiza wadau wa mazingira pamoja na wananchi kutunza uhifadhi wa mazingira kwani Tanzania imejaaliwa kuwa na utajiri wa maliasili ambapo takribani hekta milioni 48.1 ni misitu inayofanya wastani wa asilimia 55 ya eneo lote la nchi kavu.

Waziri Mkuu ametaka zoezi la kutunza mazingira kwa ajili ya maendeleo lisiwe la serikali pekee bali iwe ni zoezi la serikali kuu, serikali za mitaa, taasisi za serikali na zisizokuwa za serikali, sekta binafsi na jamii nzima kuanzia mijini mpaka vijijini.

“Kutokana na mwenendo wa hali ya mazingira nchini hatuna budi kutekeleza mipango na mikakati ya usimamizi wa mazingira ambayo ni vyema uwe shirikishi huku ukijumuisha ufuatiliaji na usimamizi thabiti na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya hali ya mazingira yetu hapa nchini,” amesema Majaliwa.

Aidha, ametoa maagizo kwa kila mamlaka za Serikali za mitaa kuanzia ngazi za mikoa, halmashauri za wilaya, kata, vijiji mpaka vitongojini ihakikishe maeneo yote yaliyoharibiwa yanarejeshwa kwa kupandwa miti na kuhakikisha inatekeleza programu ya kitaifa ya upandaji miti milioni 1.5 ili hakikisha nchi inakuwa ya kijani.

Hata hivyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jaffo amesema kampeni ya ‘Soma na mti’ imesaidia sana ongezeko la miti nchini ambapo amewapongeza wanafunzi ambao amewaita ni vinara wa kampeni hiyo mashuleni.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yamehitimishwa jijini Dodoma ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amegawa Tuzo za heshima kwa wadau wa mazingira nchini.