Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza viongozi wa wizara ya Maliasili na Utalii na Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwenda mara moja wilayani Mbarali mkoani Mbeya kufuatia taarifa za Wananchi kupigwa na kuteswa na askari wa TANAPA na Ijumaa usiku Mei 12 watoe taarifa kwake kuhusu sintofahamu inayoendelea wilayani humo.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo kufuatia Taarifa iliyotolewa na Mbunge wa Mabarali, Francis Mtega aliyemuomba Spika kusimamisha shughuli zilizo katika ratiba ya leo ya Bunge ili wabunge wajadili jambo linaloendelea jimboni kwake.
Katika maelezo yake Mtega amesema Mei 06 mwaka huu askari wa TANAPA walifika jimboni kwake na Chopa na kisha kuanza kuwapiga na kuwatesa Wananchi wake licha ya maelezo ya Serikali kuwa Wananchi hao waendelee kuishi katika vijiji vyao kama ambavyo tangazo la serikali namba 28 linavyoeleza.
Akitumia kanuni ya 54 ya Bunge, Mtega aliliomba Bunge kusimamisha shughuli zake na kujadili suala hilo lakini Spika alimpa nafasi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa maelezo kabla ya kuruhusu mjadala huo uendelee ndani ya Bunge.
Waziri Mkuu ametoa agizo la kuwataka viongozi wa juu wa wizara ya Maliasili na Utalii na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA pamoja na mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera kwenda Mbarali na kufuatilia suala hilo na kumpatia taarifa ndani ya saa 24.
Akihitimisha hoja hiyo Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amewataka Wabunge kuwa watulivu na kwamba Serikali itatoa taarifa na hatua zitakazochukuliwa baada ya taarifa hiyo kumfikia Waziri Mkuu.