Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Anthony Mavunde amewataka waajiri wote wanaoleta wafanyakazi wa kigeni kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza mpango wa urithishaji ujuzi kwa wafanyakazi wazawa kama inavyoelekezwa na Sheria ya Uratibu ya Ajira kwa Wageni Na. 1 ya Mwaka 2015
Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam katika ofisi za makao mkuu ya kampuni ya magari ya TATA wakati wa uzinduzi wa programu ya kukuza ujuzi kwa vijana inayojulikana kama SkillPro.
Vijana mafundi wa kitanzania wanapata nafasi ya kupata ujuzi nchini India wa namna ya kutengeneza magari aina ya TATA na ufundi wa jumla wa magari pamoja na uzinduzi wa gari ambalo ni gereji itakayozunguka kwenye gereji za mtaani kuwafundisha mafundi na kuwatambua kwa kuwapa vyeti vya kutengeneza magari ya TATA.
“Nawapongeza TATA kwa mpango huu wa kuwajengea ujuzi wafanyakazi wazawa, waajiri wengine waige mfano huu wa kuja na program zenye nia ya kurithisha ujuzi kwa wafanyakazi ili kupunguza utegemezi wa wafanyakazi kutoka nje ya nchi. Wale waajiri wenye wafanyakazi wageni na hawatekelezi mpango wa urithishaji wa ujuzi kwa mujibu wa sheria, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao kwa kukiuka utaratibu wa sheria,” alisema Mavunde
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TATA, Rajiv Bhushan ameeleza bayana kwamba kampuni yake imejipanga kuwawezesha vijana wa kitanzania kwa kutekeleza programu mbalimbali za mafunzo ya ufundi na kuonesha utayari wa kushirikiana na serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa ujuzi stahiki.
Akishukuru kwa niaba ya wanufaikaji wa programu hiyo, ndugu Osmund Kapinga amepongeza mafunzo yanayoendeshwa na kampuni ya TATA nchini India, ambayo yanawafanya kupata ujuzi wa ziada tofauti na ufundi. Hali ambayo imepelekea kupata nafasi za utawala ambapo amejitolea mfano yeye mwenyewe kwa kuteuliwa kuwa meneja wa Tawi la TATA Arusha.