Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, amelazimika kutoa maelezo kuhusu matukio ya mauaji yanayotokea mara kwa mara katika jamii, na kuitaka serikali kuangalia namna ya kukabiliana na matukio hayo.
Spika wa Bunge amelazimika kutoa maelezo hayo kuhusu matukio ya mauaji yanayotokana hasa na mapenzi ama watu kujichukulia sheria mkononi, mara baada ya majibu ya wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi yalitolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Chilo.
Spika Tulia ameitaka serikali kuangalia namna ambavyo itadhibiti utoaji taarifa za matukio hayo ili jamii husika pekee ndio iwe inayafahamu.
Baada ya maelezo hayo ya Spika, Waziri wa Nchi, ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene akatoa maelezo ya serikali na kukubalina na ushauri huo wa spika wa kuona namna ya kudhibiti utoaji taarifa wa matukio hayo ya mauaji katika jamii.