Wakulima wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wametakiwa kujifunza utayarishaji wa mbolea ya asili maarufu kwa jina la Mbolea Vunde itokanayo na maozo ya wanyama na mimea, ili kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani ambazo hutokana na kemikali.
Akizungumza na Wakulima wa kijiji cha Kilando, Afisa Kilimo wa mkoa wa Kigoma, James Peter amesema kuwa, utayarishaji wa mbolea Vunde husaidia kupunguza gharama za kilimo kutokana na kutumia malighafi za asili zenye uwezo mkubwa wa kuhuisha afya ya udongo kwa muda mrefu
Amesema mbolea Vunde hutumika wakati wa kupandia na baada ya hapo mkulima hawajibiki kuweka mbolea nyingine mpaka atakapovuna, na udongo kuendelea kubaki na rutuba ya kuwezesha kilimo kingine kwa muda wa miaka mitatu bila kuweka tena mbolea, tofauti na matumizi ya mbolea za viwandani.
Kwa upande wao Wakulima wa vijiji vya majaribio vya Vikonge na Isubangala wilayani Tanganyika mkoani Katavi na Kijiji cha Kajeje wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, wamesema mbolea Vunde imeonesha mafanikio makubwa katika uzalishaji wa mazao.
Wamesema baada ya kutumia mbolea hiyo shamba la hekari moja ya mahindi limetoa mavuno ya gunia 45 mpaka 50 huku hekari moja ya shamba la Maharage likitoa gunia 18 hadi 22.