Matumizi ya dawa za kulevya yapungua kwa asilimia 90

0
2134

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya nchini yamepungua kwa asilimia 90 baada ya serikali kufanikiwa kudhibiti biashara ya dawa hizo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam baada ya kufungua mkutano wa 28 wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya kutoka nchi za Afrika ujulikanao kama 28th HONLEA – Afrika.

Mkutano huo unashirikisha wajumbe zaidi ya 120 kutoka nchi 54 za Afrika na unatarajiwa kutoka na maazimio ya namna ya kutokomeza biashara ya dawa za kulevya katika mataifa hayo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika nchi hizo.

“Ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja ya kudhibiti uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya Barani Afrika. Hata hivyo ni muhimu kudhibiti njia zote zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Hata hivyo amesema kuwa Tanzania inaendelea na mikakati ya kupambana na uzalishaji wa dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na mirungi na bangi, ambayo inapandwa kwa kuchanganywa na mazao ya chakula.
Waziri Mkuu Majaliwa amewaambia washiriki wa mkutano huo wa 28 wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya kutoka nchi za Afrika kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza katika Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuanzisha vituo vya utoaji wa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya mwaka 2011.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017, jumla vituo sita vya kutolea matibabu vilianzishwa, ambapo zaidi ya waathirika Elfu sita na mia tano wa dawa za kulevya aina ya heroin walijiandikisha na kupatiwa matibabu.