Matokeo yatakayo nufaisha mkoa wa Kigoma kutokana na fainali ya Simba na Yanga

0
150

Kufanyika kwa fainali za Kombe la Shirikisho mkoani Kigoma ambako ni magharibi mwa Tanzania, kunatajwa kufungua fursa mpya za utalii na kukuza uchumi kwa wakazi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na maeneo mengine.

Akizungumza katika mahojiano.maalum na TBC mkoani Kigoma Stesheni Masta wa mkoa huo Ally Shamte amesema kuwa, kuna faida lukuki zitakazopatikana mkoani humo kutokana na kupokea wageni wengi wanaokwenda kushuhudia fainali hiyo inayokuitanisha miamba ya soka nchini Simba na Yanga tarehe 25 mwezi huu.

Shamte ameongeza kuwa, ushirikiano wa karibu baina ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), chama cha soka mkoa wa Kigoma na uongozi wa mkoa huo, umesaidia kufanikisha maandalizi ya Dabi hiyo yenye mvuto wa aina yake hapa nchini na nje ya nchi.

Akifafanua umuhimu wa Reli ya Kati, Shamte amesema huwezi kutenganisha maisha ya watu wa kigoma na reli kwa kuwa ndio tegemeo lao kubwa kiuchumi, hivyo wanafanya kila namna kuhakikisha huduma za usafiri wa abiria na mizigo unakuwa imara kila wakati

“Kila wakati Serikali na uongozi wa TRC tunahakikisha Wananchi na watumiaji wa usafiri wa reli yetu hawakwaziki kila wanapohitaji huduma yetu, maana huu ndio mgongo wa uchumi wa watu wa Kigoma.” Ameongeza Stesheni Masta huyo wa mkoa wa Kigoma

Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam ilianza kujengwa na Mjerumani mwaka 1906 na kukamilika mkoani Kigoma mwaka 1914 ikiwa na urefu wa Kilomita 1, 251.

Reli hiyo imekuwa mkombozi wa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika ukanda wa Magharibi mwa Tanzania na nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).