Matokeo ya kidato cha nne yatangazwa

0
1544

Jumla ya watahiniwa 322, 965 ambao ni sawa na asiliamia 78.38 ya watahiniwa 426,988 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018 wamefaulu mitihani yao.

Akitangaza matokeo  hayo jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) Dakta Charles Msonde amesema kuwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kimeongezeka kutoka asilimia 77.09 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 78.38 mwaka 2018.

Dkt Msonde amezitaja shule kumi zilizofanya vizuri ambazo zina idadi ya watahiniwa zaidi ya arobaini kuwa ni St Francis Girls ya mkoani Mbeya, Kemebos ya mkoani Kagera, Marian Boys ya mkoani Pwani, Ahmes ya mkoani Pwani, Canossa ya mkoani Dar es salaam, Maua Seminary  ya Kilimanjaro, Precious Blood ya mkoani Kilimanjaro, Marian Girls ya mkoani Pwani,  Bright Future Girls ya mkoani Dar es salaam na Bethel Sabs Girls ya mkoani Iringa.

Shule zilizofanya vibaya katika mtihani huo ni Pwani Mchangani ya Kaskazini Unguja, Ukutini ya Kusini Pemba, Kwediboma ya mkoani Tanga, Rwemondo ya mkoani Kagera, Namatula ya mkaoni Lindi, Kijini ya Kaskazini Unguja, Komkalakala ya mkoani Tanga, Kwizu ya mkoani Kilimanjaro, Seuta ya  mkoani Tanga na Masjid Qubah Muslim ya mkoani Dar es salaam.

Dkt Msonde ameongeza kuwa hali ya ufanyikaji wa mtihani huo wa kidato cha nne nchini mwaka 2018 ni nzuri kwa kuwa ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu na kwa kuzingatia kanuni za mitihani.

Hata hivyo amesema kuwa shule ya sekondari ya  Tumaini Lutheran Seminary iliyopo wilayani Malinyi mkoani  Morogoro imefutiwa matokeo ya watahiniwa wote,  pamoja na kufungwa kwa kituo hicho kutokana na kufanya udanganyifu.