Matengenezo ya barabara iliyokatika yaendelea

0
291

Kazi ya kutengeneza sehemu ya barabara iliyokatika kwenye eneo la Kiyegeya (Magubike) wilayani Kilosa katika barabara kuu ya Morogoro – Dodoma imeanza kwa kuweka vifusi pamoja na mawe.

Habari kutoka mkoani Morogoro zinaeleza kuwa mbali na kazi hiyo ya kuweka vifusi na mawe, madaraja mawili ya chuma yanaendelea kuunganishwa ili kufungwa kwenye eneo lilipokatika.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa ambaye ametembelea eneo hilo ameeleza kuwa, kazi hiyo ya kuunganisha madaraja mawili ya chuma inafanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wakati matengenezo hayo yakiendelea, baadhi ya abiria waliokwama katika  barabara hiyo ya Morogoro – Dodoma wamesema kuwa wanapata adha kubwa kwa kukaa kwa muda mrefu  kwenye eneo hilo ambalo halina huduma muhimu.

Kukatika kwa daraja la mto Kiyegeya kumesababisha kukwama kwa usafiri kati ya mikoa ya Morogoro na Dodoma na kuwalazimu wasafiri kutumia viunganisho mbadala ikiwemo barabara ya Morogoro – Iringa – Dodoma na mikoa mingine ya kanda ya kati katika hipindi hiki ambapo matengenezo yanaendelea.