Uongozi wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera umesitisha masomo katika shule ya sekondari ya Bukoba baada ya mabati ya baadhi ya majengo yake kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro amesema baadhi ya wanafunzi watahamishiwa katika sule za sekondari za Ihungo na Omumwani ambazo zina nafasi ya kuwahifadhi wanafunzi hao.
Mvua iliyoambatana na upepo mkali ilianza majira ya saa kumi na moja alfajiri imesababisha kuezuliwa kwa mapaa katika jengo la utawala, madarasa manane ya kidato cha kwanza hadi cha tatu pamoja na maktaba katika shule ya sekondari Bukoba mkoani Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Gaguti amesema serikali mkoani humo itahakikisha inashirikiana na uongozi wa wilaya kurejesha miundombinu ya shule hiyo katika hali yake ya kawaida.
Wanafunzi 97 wa kidato cha tano na sita wanatarajiwa kuhamishiwa katika shule ya sekondari Ihungo Ilhali wanafunzi 751 wa kidato cha kwanza hadi cha nne wakitarajia kuhamishiwa katika shule ya sekondari Omumwani.