Mashirika 187 yapewa siku Sitini kuwasilisha Gawio Serikalini

0
220

Rais John Magufuli ametoa muda wa siku Sitini kwa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 187 ambazo zimeshindwa kuwasilisha Gawio, Michango na ziada Serikalini ziwe zimefanya hivyo.

Rais Magufuli ametoa muda huo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, wakati akipokea Gawio, Michango na ziada ya Serikali kutoka Mashirika, Kampuni na Taasisi mbalimbali zinazomilikiwa na Serikali.

Amesema kuwa haiwezekani Serikali ikawa imewekeza takribani Shilingi Trilioni 56 kwa ajili ya kuendesha Mashirika na Kampuni zake 266, halafu zinazokuja kutoa Gawio ni 79 tu.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kila mwaka baadhi ya Mashirika na Taasisi za Umma zimekua hazitoa Gawio Serikalini kwa madai kuwa zinajiendesha kihasara, wakati zina vitega uchumi pamoja na Viongozi.

Amesema kuwa zitakapomalizika siku hizo Sitini na Mashirika ama Kampuni hizo zitakuwa hazijawasilisha Gawio Serikalini, Bodi za Mashirika hayo ziandike barua za kujivunja zenyewe na Wakuu wa Mashirika hayo wajihesabu kuwa hawapo kwenye nyadhifa hizo.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa, kwa bodi ambazo uteuzi wake unafanywa na yeye, zijihesabu kuwa zimevunjika.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli amepokea Shilingi Trilioni 1.05 kama Gawio kutoka Mashirika, Kampuni na Taasisi mbalimbali za Umma.