Mashine ya kukoboa mpunga yazinduliwa Mvomero

0
152

Waziri wa Kilimo, – Japhet Hasunga amelipongeza Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), Serikali ya Venezuela pamoja na Halmashauri za wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero zote za mkoa wa Morogoro kwa kutekeleza mradi wa Ubia wa Maendeleo ya Mifumo ya Uzalishaji Endelevu wa Mpunga Afrika chini ya Jangwa la Sahara.

Waziri Hasunga ametoa pongezi hizo wilayani Mvomero wakati akizindua mashine ya kukoboa mpunga katika kijiji cha Mkindo, ambayo ni miongoni mwa mashine kubwa Nne zilizonunuliwa na kusimikwa kupitia mradi huo.

Pamoja na mambo mengine, mradi huo wa Ubia wa Maendeleo ya Mifumo ya Uzalishaji Endelevu wa Mpunga Afrika chini ya Jangwa la Sahara, ulikuwa na jukumu la kuwafundisha vijana kilimo shadidi cha mpunga ambacho kinatumia mbegu kidogo zenye ubora na maji kidogo huku kikiwahakikishia Wakulima mavuno zaidi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashine hizo Waziri Hasunga amesema kuwa, lengo la Serikali ni kuendelea kushirikiana na Shirika hilo la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, Serikali ya Venezuela na  Halmashauri za wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero zilizopo mkoani Morogoro ili kuhakikisha Wakulima katika halmashauri hizo Tatu wanatunza mazao yao na wanapunguza upotevu wa mazao yao baada ya mavuno pamoja na kuyaongezea thamani.