Mashine ya kuchenjulia dhahabu unayomilikiwa na kampuni ya OSA ya wilayani Songwe mkoani Songwe imefungiwa kutoa huduma, baada ya kutuhumiwa kuwaibia wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu pindi wanapokwenda kuchenjua.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa TBC mkoani Songwe, Afisa Madini Mkazi wa mkoa huo Mhandisi Laurent Mayala amesema wameifungia mashine hiyo baada ya kufanya uchunguzi na kubaini kuwa ina mapungufu kadhaa.
Mhandisi Mayala amesema uchunguzi wa tuhuma hizo wameliachia Jeshi la Polisi.
Hata hivyo amesema kwa sasa wamejipanga kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika mashine zote zinazochenjua dhahabu ili kubaini kama zipo zingine zinazojihusisha na wizi wa namna hiyo, na endapo zitabainika hatua za kisheria zitachukuliwa.