Serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Balozi wa Marekani nchini wa kupambana na Virusi vinavyosababisha Ukimwi na Ukimwi, umetoa msaada wa Shilingi Milioni 500 kwa Asasi 11 za kiraia, kwa lengo la kupambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi hapa nchini.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dkt Inmi Patterson amekabidhi fedha hizo jijini Dar es salaam, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kupambana na Virusi vinavyosababisha Ukimwi na Ukimwi kwa asasi hizo, ikiwa ni muendelezo wa Ubalozi huo kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi kwa jamii ya Kitazania.
Balozi Patterson amesema kuwa, mwaka huu wamepokea maombi kutoka Asasi 224 katika utekelezaji wa miradi ya Ukimwi, lakini Asasi 11 pekee ndizo zimefanikiwa kupata fedha ambazo zitafanya kazi kwenye miradi ya Vijana, akina Baba, Wanawake, Watoto na Jamii za wafugaji.
Mfuko huo wa Balozi wa Marekani hapa nchini wa kupambana na Virusi vinavyosababisha Ukimwi na Ukimwi, umekua ukitoa fedha hizo kwa mwaka wa 16 hivi sasa, ambapo tayari umetoa Shilingi Bilioni 4.6 kuzipatia asasi za kiraia zaidi ya 130.
Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa mradi huo kwa mwaka huu wameeleza kuwa, fedha hizo zitawasaidia kuongeza mapambano dhidi ya Virusi vinavyosababisha Ukimwi na Ukimwi.