Mapingamizi ya kina Mbowe yagonga mwamba

0
146

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo mkoani Dar es Salaam, imetupilia mbali mapingamizi saba ya upande wa utetezi katika shauri dogo ndani ya kesi ya msingi namba 16 ya mwaka 2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo siku 13 zilizopita, shahidi namba 8 ASP Jumanne wakati akitoa ushahidi wake aliieleza mahakama namna alivyopewa kazi ya kuandika maelezo ya mshtakiwa wa tatu Mohamed Ling’wenya katika kituo Kikuu cha polisi, Dar es Salaam

Baada ya kutoa maelezo hayo, aliomba maelezo hayo yapokelewe mahakamani kama sehemu ya ushahidi ambapo upande wa utetezi uliyapinga kwa kutoa sababu saba ambazo mahakama iliwataka kuwasilisha hoja hizo kwa njia maandishi.

Moja ya sababu zilizotajwa hapo awali na upande wa utetezi, ni kwamba mshtakiwa namba tatu hakuwahi kupelekwa kituo Kikuu cha polisi, Dar es Salaam na wala hakuchukuliwa maelezo yoyote bali alipelekwa kituo cha polisi Tazara na baadaye Mbweni baada ya kukamatwa huko Rau Madukani mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kula njama ya kutenda vitendo vya kigaidi katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata hivyo Jaji Joachim Tiganga wa mahakama hiyo ameeleza kwamba hoja zilizotolewa na Mawakili wa utetezi ukiongozwa na Peter Kibatala juu ya mshtakiwa namba tatu Mohamed Ling’wenya hayana mashiko.

Jaji Tiganga amesema mshtakiwa Mohamed Ling’wenya hakuwa na maelezo ya kutosheleza kuthibitisha kwamba hakupelekwa kituo Kikuu cha polisi, Dar es Salaam na wala hakuweza kutoa maelezo ya kutosha juu ya kutishiwa kwake ili aweze kutoa maelezo kwa Afande Ricardo Msemwa.

Kutolewa kwa hukumu hiyo ya shauri dogo, kunaifanya mahakama hiyo sasa kuendelea na kesi ya msingi.

Baada ya Jaji Tiganga kutoa uamuzi huo, mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi tarehe 15 mwezi huu ambapo shahidi wa nane wa upande wa mashtaka atamalizia kutoa ushahidi wake alipoishia baada ya kuibuka kwa kesi ndogo.