Mapigano ya wakulima na wafugaji yazuka Mkuranga

0
2575

Watu Sita wamejeruhiwa baada ya kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Kondomwelanzi kilichopo kwenye eneo la mpaka wa wilaya za Mkuranga na Kisarawe mkoani Pwani.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga , -Filberto Sanga amesema kuwa mapigano hayo yamezuka baada ya kundi la wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima na kuharibu mazao.

Amesema kuwa baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Mkuranga kupata taarifa hizo, askari walitumwa katika eneo la tukio kwa lengo la kuwasaka wafugaji waliosababisha mapigano hayo ambao hawajapatikana na jitihada za kuwatafuta zinaendelea.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mkuranga ameongeza kuwa ili kuzuia kutokea kwa matukio kama hayo, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mkuranga itaenda katika kijiji hicho kwa lengo la kuzungumza na wakazi wake ili kukubaliana namna ya kufanya pindi yanapojitokeza matukio ya aina hiyo na si kuingia katika mapigano.

Sanga amefafanua kuwa mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika kijiji hicho cha Kondomwelanzi yamesababishwa na ongezeko la mifugo hasa ng’ómbe baada ya wafugaji wengi kuondolewa katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya jirani ya Kisarawe.