Maonesho ya Karibu Utalii Kusini yazinduliwa

0
247

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Akson amesema kuwa, uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege na barabara kwa Nyanda za Juu Kusini, utachangia kukuza utalii.

Dkt Tulia Akson ametoa kauli hiyo wakati uzinduzi wa maonesho ya Karibu Utalii Kusini, yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa – Kilolo mkoani Iringa na kushirikisha Taasisi za Umma na za Binafsi.

Amewaeleza Washiriki wa maonesho hayo kuwa, amefarijika kupata taarifa kuwa kuna matengenezo makubwa ya kiwanja cha ndege cha Iringa, ili kiweze kuhudumia ndege kubwa zaidi ya Bombardier ambayo inabeba abiria 72.

Naibu Spika huyo wa Bunge amewataka wakazi wa Nyanda za Juu Kusini kuwa wabunifu kwa kuvutia Watalii kutembelea vivutio vilivyopo, ikiwemo Milima, Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Udzungwa, Katavi na Kitulo, Kimondo cha Mbozi, Maporomoko ya Maji ya Kalambo na Ziwa Ngosi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, -Ally Hapi amemshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ya kiwanja hicho cha Iringa.