Manyoni kupata gari la wagonjwa

0
1987

Serikali imeahidi kupeleka gari ya kubeba wagonjwa  katika hospitali ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida ili kutatua tatizo linaloikabili wilaya hiyo hasa vifo vinavyotokana na uzazi.

Ahadi hiyo  ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alipotembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea hali ya utoaji huduma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Dkt Ndugulile amefikia uamuzi wa kutoa ahadi hiyo baada ya kusikiliza kero za wananchi wanaotumia hospitali hiyo ambao wamesema kuwa gari la wagonjwa lingeweza kuepusha vifo vya akina mama wajawazito na watoto pamoja na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.

“Naomba niwaahidi wananchi wa Manyoni, serikali imeagiza magari ya kubebea wagonjwa ambayo yanaweza kufika mwezi Disemba mwaka huu, hivyo nitahakikisha katika mgao wa magari hayo basi na hospitali hii ya wilaya  inapata gari moja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa hapa”, amesema Dkt Ndugulile.

Naye Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Manyoni Dkt Atupele Mohamed amesema kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa majengo kikiwemo chumba cha huduma za uzazi ambapo uwezo wake kwa mwezi ni  kuzalisha akina mama 90 lakini kwa sasa wanazalisha  wastani wa akina mama 400.