Mamlaka zaagizwa kuyabaini majengo hatarishi

0
187

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduz Dkt Hussein Mwinyi ameziagiza Mamlaka zote zinazoshughulika na nyumba zilizopo Mji Mkongwe kuhakikisha zinayabaini na kuyafunga majengo yote yaliyo kwenye hali isiyoridhisha ili kunusuru maafa yanayoweza kujitokeza.

Dkt Mwinyi ametoa agizo hilo baada ya kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya kuanguka kwa sehemu ya jengo la kihistoria la Beit Al Ajaib iliyotokea hapo jana, wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Zanzibar.

Amesema ni vema kazi ya kuyabaini majengo hayo ya zamani yaliyokuwa katika hali isiyoridhisha ikafanyika haraka, kwani hataki kusikia tukio kama hilo linatokea tena.

Ajali hiyo ya kuanguka kwa sehemu ya jengo la kihistoria la Beit Al Ajaib imesababisha vifo vya watu wawili ambao tayari miili yao imekwishaondoleea katika vifusi vya jengo hilo na wengine wanne wamejeruhiwa.

Zoezi la kuondoa kifusi cha jengo hilo ambalo lilianguka wakati likifanyiwa ukarabati bado linaendelea.