Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amesema kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo na mchango wake katika maendeleo ya Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuboreshwa.
Akizungumza na Wanachama wa CCM mkoa wa Tabora Kinana amezungumzia sekta ya kilimo hasa hatua zinazochukuliwa na Serikali kutatua changamoto za Wakulima.
“Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameeeleza yanayoendelea kwenye kilimo, amezungumzia mambo mbalimbali ya kilimo, kama hujamsikia na ukasikiliza kero peke yake unapata hisia kuna kero hazishughulikiwi, lakini ukisikiliza kwa makini unaona kuna kazi inafanyika, kuna ufumbuzi unaotolewa kwa matatizo hayo…….
Rais Samia Suluhu Hassan wakati anachukua nchi hii wizara ya Kilimo ilikuwa ikipata shilingi Bilioni 260, lakini leo inapata shilingi Trilioni moja,” Amesema Kinana.
Amefafanua kuwa miradi mingi ama ilisimama au ilipuuzwa, lakini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza maafisa ugani wameajiriwa, vitendea kazi vipo vya kutosha, pembejeo zinatolewa kwa ruzuku kutoka Serikalini na ni kwa mazao yote.