Aliyewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika,- Mama Getrude Mongella ameitaka Serikali kuwapatia Wanawake wa Tanzania Kiwanda cha kubangua Korosho ili wajitegemee badala ya kuendelea kusubiri kuajiriwa kwa kazi za kubangua Korosho kila siku.
Akizungumzia uzoefu wake kuhusu maisha ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati wa Kongamano la kumbukumbu ya miaka Ishirini ya kifo cha Baba wa Taifa linalofanyika Mkoani Lindi, Mama Mongella amesema kuwa wakati umefika kwa Wanawake kupewa nafasi ya kujitegemea na kuacha kutegemea kuajiriwa kama vibarua wa kubangua Korosho.
Mama Mongella ambaye pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali nchini kwa nyakati tofauti amesema kuwa, viwanda vilijengwa na Hayati Mwalimu Nyerere, hivyo Wanawake nao wakumbukwe kwa kupewa Kiwanda na waanze kujitegemea ikiwa ni njia ya kuwafanya wamkumbuke.
Mwanasiasa huyo ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Ukerewe mkoani Mwanza amesema kuwa, Wanawake wamesahauliwa katika urithi wa Hayati Mwalimu Nyerere, hivyo ameomba wakumbukwe walau kupewa Kiwanda cha kubangua Korosho ili wakiendeshe na kuuza bidhaa za Korosho nje na ndani ya nchi.
