Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Alex Malasusa amesema kuwa uongozi wa Hayati Dkt. John Magufuli ulikuwa wa pekee kwani ulikuwa tofauti na viongozi wengi wa Afrika.
Akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu ambayo imefanyika kitaifa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CCT UDSM Chaplaincy), Dkt. Malasusa amesema kuwa Dkt. Magufuli hakuwa mwanasiasa, bali alikuwa kiongozi ambaye alitenda mambo, siyo tu kuishia kuongea.
“Uongozi wa Magufuli ulikuwa wa pekee, nasi kama Watanzania tuna cha kujifunza,” amesema Malasusa katika mahubiri yake.
Amesema kuwa rafiki yake amewahi kumwambia kuwa “Afrika ina wanasiasa wengi sana, lakini kwa bahati mbaya ina viongozi wachache sana. John Pombe Magufuli wa Tanzania alikuwa kiongozi na ndiyo maana Watanzania waliomboleza.”
Ameeleza kuwa Dkt. Magufuli alikuwa fahari ya Waafrika na kwamba kwa muda mfupi ameweza kufanya kitu ambacho labda kisingefanyika au ingechukua muda mrefupi kufanyika.
“Hatuhitaji siasa tu, lakini tuhahitaji uongozi,” ameeleza Malasusa huku akiongeza kuwa maneno yamekuwa mengi huku utendaji kazi ukiwa hafifu sana.
Leo Aprili 2, 2021 ni siku ya 17 ya maombolezo ya kifo cha Dkt. Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17 na kuzikwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita Machi 26.