Halmashauri ya wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, imeagiza kuvunjwa kwa makundi yote Sogozi(WhatsApp Groups) ambayo yamekua yakitumiwa na Watendaji wa Idara ya Elimu wilayani humo kwa ajili ya kutoa na kupokea taarifa za kiutendaji na kitaalamu.
Barua iliyotolewa katika siku za hivi karibuni na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo imeeleza kuwa, makundi hayo Sogozi yamekua yakitumiwa na Watendaji hao kutoka taarifa za kijamii na kielimu kama vile Walimu Wakuu waliovuliwa madaraka na wengine walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali.
Kwa mujibu wa barua hiyo, hatua za kinidhamu zitachukiliwa dhidi ya viongozi wa makundi hayo endapo wataendelea kukaidi agizo hilo.
Halmashauri ya wilaya ya Chemba imetoa agizo hilo katika kipindi hiki ambapo Wanafunzi wa Darasa la Saba wanatarajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi tarehe 11 na 12 mwezi huu.
Mwaka 2018 shule za zote Halmashauri ya wilaya ya Chemba zilifutiwa matokeo ya mitihani ya Darasa la Saba baada ya kubainika kuwepo kwa vitendo vya udanganyifu, vitendo vilivyodaiwa kufanywa kupitia makundi Sogozi(WhatsApp Groups).