Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, -Paul Makonda ameahidi kuchangisha Shilingi Bilioni Moja kusaidia matibabu ya moyo kwa Wananchi wasio na uwezo wa kugharamia matibabu ya ugonjwa huo.
Mbali na ahadi hiyo, Makonda pia ameahidi kuendelea kusaidia watoto Kumi kila mwezi kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo mpaka kufikia mwishoni mwaka huu watoto Sitini watanufaika na msaada huo wa Mkuu wa mkoa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kambi ya upasuaji wa magonjwa ya Moyo kwa watoto wadogo inayofadhiliwa na Ubalozi wa Falme za Kiarabu hapa nchini, Makonda amesema kuwa ameamua kutoa msaada huo baada ya kuona mahitaji makubwa ya watoto wanaotakiwa kupatiwa matibabu ya moyo lakini hawana uwezo wa kugharamia matibabu hayo.
Zoezi hilo limeanza mwezi Julai mwaka huu, ambapo mpaka sasa jumla ya watoto Thelathini wamekwishafanyiwa upasuaji na pia kupatiwa matibabu ya Moyo kupitia mpango huo huku lengo likiwa ni kutoa huduma hiyo kwa watoto Sitini ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Mbali na Kampeni hiyo, pia Makonda ameahidi kufanya harambee kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu ili kupata Shilingi Bilioni Moja kusaidia watoto zaidi huku akimshukuru Balozi wa Falme za Kiarabu hapa nchini Khalifa Abdulrahman Al- Mazzooqi kwa kuendelea kusaidia katika matibabu hayo.
Aidha Makonda amesema kuwa yeye kwa kushirikiana na Balozi Al –Mazzooqi watawalipia Bima ya Afya watoto Mia Tano na hasa wanaopatiwa matibabu ya moyo ili waendelee kupatiwa matibabu kwa kutumia kadi zao za Bima ya Afya.
Kwa Upande wake Balozi wa Falme za Kiarabu hapa nchini Khalifa Abdulrahman Al- Mazzooqi amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha watoto hao wanapatiwa matibabu.