Makandarasi wazawa wametakiwa kuzisimamia kampuni zao kwa ufasaha kwa kufuata sheria za ulipaji kodi kwa wakati, na kufanya kazi kwa weledi kwa kutumia wataalam stahiki katika sekta mbalimbali.
Akizungumza jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo yenye lengo la kuwajenga Makandarasi wazawa kibiashara, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Rhoben Nkori amesema, lengo mojawapo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa makandarasi kuhusu mvutano uliopo baina yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Nimefurahi kuona kwamba moja ya mada itakayofundishwa ni kuhusu masuala ya kodi kwa Makandarasi, hii itatusaidia kupunguza matatizo makubwa sana kati ya Wakandarasi na TRA,” amesema Nkori.
Amesema kampuni nyingine hutumika kufanya kazi kwa majina ya wamiliki wengine, hali inayosababisha mvutano pindi kazi inapoenda kukaguliwa na TRA kupitia CRB, na hivyo kuwataka wamiliki wa kampuni kusimamia vema kampuni zao ili kuepuka changamoto hizo.
Aidha, Nkori ametoa wito kwa Makandarasi wa ndani kusimamia kwa weledi kampuni zao kwa kutumia wataalam stahiki na kutekeleza miradi kwa viwango vyenye ubora, ili Watanzania waweze kunufaika na miradi hiyo.
“Mafunzo haya yanayoendana na biashara yawajengee uwezo wa kuwa tofauti katika soko maana biashara zote zina ushindani na ili uweze kuwa tofauti unatakiwa kuwa na mbinu sahihi na weledi,” asema Msajili huyo wa CRB.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayotolewa na
Bodi ya Usajili wa Makandarasi
yanashirikisha Makandarasi kutoka sehemu mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo makandarasi hao katika kutekeleza majukumu yao.