MAKAMU WA RAIS AWAKUMBUKA WAHITAJI SIKUKUU YA KRISMASI

0
156

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 24 Desemba 2021 amekabidhi zawadi mbalimbali za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya katika kituo cha kulea watoto yatima cha Poloni kilichopo Kondoa mkoani Dodoma.

Akikabidhi kwa niaba ya Makamu wa Rais, msaidizi wa Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Emma Liwenga amesema zawadi hizo ni katika kukidhi mahitaji ya watoto hao kipindi hiki cha sikukuu. Amesema Makamu wa Rais ametuma salamu za Upendo na kuwaomba watoto hao kukua katika maadili.

Aidha Dkt Emma amesema Makamu wa Rais amewashukuru waangalizi wa watoto hao kwa kujitoa kwao kuwalea katika maadili mema na kuomuomba Mungu kuendelea kuwabariki Masista na wahudumu wengine katika malezi yao kwa watoto hao.

Kituo hicho cha Poloni kilianzishwa Mwaka 1947 na mpaka sasa kina jumla ya watoto 46 ambao wanapokelewa kuanzia umri wa siku moja tangu kuzaliwa.

Zawadi zilizokabidhiwa ni pamoja na Mchele, Unga wa Ngano, Sabuni, Sukari, Mafuta, vinywaji pamoja na mbuzi wawili.