Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ateta na Waziri Ummy Mwalimu

0
154

Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar, – Hemed Suleiman Abdallah amesema ni vema changamoto za Muungano zinapojitokeza zipatiwe ufumbuzi wa haraka kupitia vikao vya pamoja baina ya  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ameyasema hayo wakati wa kikao baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Ummy Mwalimu aliyefika ofisini kwake huko Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha.

Amempongeza Waziri Ummy Mwalimu kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kumuahidi kumpa ushirikiano katika kuratibu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa mustakabali wa Taifa.

“Naamini kuletwa katika Wizara hii utapata fursa nzuri ya kusimamia masuala ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali na Taasisi zetu kwa maslahi ya Watanzania wote, nina imani kubwa na utendaji wako, sina shaka kabisa,” amesisitiza Makamu huyo wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah.

Kwa upande wake Waziri Ummy Mwalimu amesema ana dhamana ya kusimamia masuala ya Muungano na Mazingira, hivyo atayasimamia masuala hayo ipasavyo.

“Napenda kukuhakikishia kuwa nitafanya kazi kwa karibu na Dkt Khalid Waziri mwenzangu katika kuhakikisha tunaimarisha Muungano wetu na kuendelea kushirikiana hata katika masuala ya mazingira kwa kuwa hayana mipaka,” amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy Mwalimu yuko Visiwani Zanzibar kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na pande zote mbili za Muungano.