Majina ya Viongozi mbalimbali walioteuliwa na Rais Magufuli

0
288

Rais John Magufuli, leo amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa, katika uteuzi huo Rais Magufuli amemteua Loata Sanare kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Dkt Kebwe Stephen ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Rais Magufuli amemteua Mussa Maselle kuwa Mkuu wa wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, ambapo kabla ya uteuzi huo Maselle alikuwa Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Tixon Nzunda ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) aliyekuwa akishughulikia Elimu.

Wengine ni Dkt Ally Possi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kabla uteuzi huo alikuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata anakua Naibu Wakili Mkuu wa Serikali ambapo awali alikuwa Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Mary Maganga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Utawala ambapo kabla ua uteuzi huo alikuwa Kamishna wa Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mhandisi Anthony Sanga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kutoka nafasi ya awali ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Jiji la Mwanza, Alphayo Kidata yeye anakua Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara kuchukua nafasi ya Dkt Jilly Maleko ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Katika uteuzi huo, Mhandisi Emmanuel Kalobelo anakua Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro ambapo kabla ya hapo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Cliford Tandali ambaye amestaafu na Khatibu Kazungu anakua Katibu Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro na kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na anachukua nafasi ya Mhandisi Aisha Amour ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Wateule hao wote wataapishwa Jumapili Septemba 22, saa Tisa alasiri Ikulu jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi,
Rais Magufuli pia amefanya uhamisho wa Wakuu wa wilaya wawili ambapo aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Tarime mkoani Mara Mhandisi Charles Kabeho amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi Mtemi Simeoni anakua Mkuu wa wilaya ya Tarime.

Uhamisho mwingine ni wa Naibu Makatibu Wakuu wawili ambapo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nicholaus Mkapa amehamishwa na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabunduguru amehamishwa na kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI anayeshughulikia Elimu.

Kwa upande wa Mabalozi, Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Mabalozi 12 watakaoiwakilisha Tanzania katika vituo vya Abu Dhabi (Falme za Kiarabu),lBujumbura (Burundi), Brussels (Ubelgiji), Cairo (Misri), Harare (Zimbabwe), Kuwait City (Kuwait), Pretoria (Afrika Kusini), Riyadh (Saudi Arabia), Tokyo (Japan), Umoja wa Mataifa (Geneva Switzerland), Umoja wa Mataifa (New York Marekani) na Abuja (Nigeria).

Walioteuliwa kuwa Mabalozi kwa ajili ya vituo hivyo ni Mohammed Mtonga ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Mstaafu, Jilly Maleko aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Dkt Benson Bana ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Meja Jenarali Mstaafu Anselm Bahati na Profesa Emmanuel Mbennah ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu cha Mtakatifu John.

Wengine ni Maimuna Tarishi ambaye ni Katibu Mkuu Mstaafu, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi Katibu Mkuu Mstaafu, Ali Jabir Mwadini ambaye ni Kansela Mkuu, Ubalozi Mdogo wa Tanzania-Dubai, Dkt Modestus Kipilimba Mkurugenzi Mkuu Mstaafu Idara ya Usalama wa Taifa, Jestas Nyamanga ambaye ni Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Kennedy Gastorn ambaye ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ushauri wa Kisheria wa Asia na Afrika yenye Makao Makuu yake New Delhi, -India.

Tarehe ya kuapishwa kwa Mabalozi hao na vituo vyao vya kazi itatangazwa baada ya taratibu za kidiplomasia kukamilika.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amewapandisha vyeo na kuwateua Maafisa Watatu kuwa Mabalozi.

Wateule hao ni Stephen Mbundi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi, Siasa na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ali Sakila Bujiku ambaye ni Msaidizi wa Rais na Dkt Mussa Lulandala ambaye ni Msaidizi wa Rais.

Mabalozi Wateule hao wataendelea kutekeleza majukumu yao hapahapa nchini na wataapishwa Jumapili Septemba 22, alasiri Ikulu jijini Dar es Salaam.