Majeruhi wengine saba wa ajali ya moto wafariki Muhimbili

0
302

Majeruhi saba kati ya 32 wa ajali ya moto waliokuwa wanatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo Agosti 15 na kufanya idadi waliofariki hadi sasa kufikia 21 huku wanaoendelea na matibabu wakiwa 25, kati ya hao 16 wapo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na 9 wapo katika wodi ya wagonjwa wa kawaida kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Agosti 15, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili-MNH, Aminiel Aligaesha, amesema hadi jana watu sita walikuwa wamefariki na tayari miili yao imesafirishwa mkoani Morogoro ndugu zao baada ya ndugu zao kujitokeza kuwachukua.

“Serikali imeahidi wanaozikwa Morogoro itagharamia mazishi lakini kwa wanaotaka kwenda Mikoa mingine kama Moshi, Tanga wanajigharamia wao ila serikali itatoa sanda na sanduku tu,” amesema.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro Jumamosi Agosti 11, na kusababisha vifo vya watu 89 na majeruhi zaidi ya 70.