Majaliwa : Tutasimamia madai ya madereva na haki za waajiri

0
120

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, serikali itahakikisha inaendelea kusimamia madai ya madereva pamoja na haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva wa malori.

Amesema lengo ni kuhakikisha madereva wanaendelea na ajira zao, na wanapata maslahi yao kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali itasimamia haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva, ili wasije wakawajibika na vitu ambavyo haviko kwenye sheria za nchi.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo mkoani Dodoma wakati akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni na Makatibu wakuu wa wizara hizo, pamoja na Mkuu wa jeshi la polisi nchini Camilius Wambura.

Waziri Mkuu ametumia kikao hicho kukitaka chama cha madereva nchini kiruhusu huduma za usafirishaji ziendelee kutolewa wakati serikali ikiendelea kushughulikia masuala yao.

“Serikali haitaridhika kuona madereva wanalalamika kila siku na pia si vizuri waajiri wakabebeshwa mizigo iliyo nje ya sheria.” amesema Waziri Mkuu

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kililenga kujadili suala la mgomo wa madereva wa malori.