Majaliwa : Tumieni urithi wa ukombozi kujikomboa kiuchumi

0
178

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka jamii kuutumia urithi wa ukombozi uliopo nchini kujikomboa kiuchumi na kifikra.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kutambua na kuenzi mchango anuai wa historia ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika na kikao kazi cha maafisa utamaduni na michezo.

Amesema kuwa ni vema jamii ambazo zinatumia au zinamiliki maeneo au miundombinu ya urithi wa ukombozi wa Afrika ikavitunza na kupata ushauri wa kitaalamu wa kuanzisha makumbusho na kuvutia utalii katika eneo hilo ili kujiongezea kipato.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa, jukumu la kuhifadhi na kulinda urithi wa ukombozi uliopo ni la kila mmoja, ili vizazi vijavyo viweze kujifunza na kuendeleza na kuongeza kuwa ” Hakuna Taifa litahifadhi historia ya kweli ya kwetu isipokuwa sisi wenyewe.”

Waziri Mkuu Majaliwa pia ameagiza makundi yote au mtu yoyote ambaye ana mali za urithi wa ukombozi aviwasilishe katika makumbusho ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika iliyopo mkoani Dar es salaam, ili vihifadhiwe kitaalamu visije vikapotea.

Ameitaja mikoa ya Lindi, Ruvuma Mtwara na Mbeya kuwa wa kwanza kunufaika na zao la Utalii wa kiukombozi

Kwa kutambua mchango wa lugha ya Kiswahili duniani, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania kutambua umuhimu wa Lugha ya Taifa .

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema lengo la kongamano hilo ni kuelimisha umma umuhimu wa kujikomboa kiuchumi na kifikra kupitia uhifadhi na utangazaji wa zao la utalii wa kiukombozi.

Kauli mbiu ya Kongamano hilo la kutambua na kuenzi mchango anuai wa historia ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika
ni “Urithi wa Ukombozi, Fahari ya Afrika”.