Majaliwa : Fanyeni mazoezi kujiepusha na maradhi

0
250

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kujijengea utaratibu wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, ili wajiepushe na maradhi pamoja na kuimarisha afya ya mwili na akili.

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo mkoani Dodoma wakati akizindua Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu.

Bonanza hilo lililopewa jina la “CRDB Bank Pamoja Bonanza”, limefanyika katika uwanja wa Jamhuri.
 
“Bonanza hili la leo limeandaliwa kwa ajili ya kutuhamasisha sisi Wafanyakazi umuhimu wa mazoezi katika kujenga na kuimarisha afya zetu na litatusaidia kuboresha utendaji wetu sehemu za kazi. Kama mnavyofahamu wengi tumekuwa wahanga wa magonjwa yasiyoambukiza.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema magonjwa hayo ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya vilevi kama sigara na pombe, kutoshiriki mazoezi au shughuli za nguvu na kutozingatia lishe bora yamekuwa chanzo cha gharama kubwa za afya kwa Serikali na kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa.
 
“Nitoe rai kwa washiriki na Watanzania kwa ujumla kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu na kuzingatia mlo sahihi kwa ajili ya kujikinga na maradhi hayo kwani siku zote kinga ni bora kuliko tiba na tuendelee kuunda vikundi vya mazoezi ya ukakamavu (Jogging) na kushiriki matamasha mbalimbali ya michezo.”amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema bonanza hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza juu ya kuwaleta watu pamoja na kushirikiana katika kujenga uchumi wa Taifa.