Majaliwa: Bwawa la Umeme la Nyerere litakamilika

0
377
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua kazi ya ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere wilayani Rufiji, Aprili 10, 2021.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kuwa mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere utakamilika kwa wakati (Juni 2022) kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo.

Waziri Mkuu amesema hayo katika ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika mradi huo na kueleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa ikiwemo ujenzi wa tuta la bwawa hilo litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.

Amesema kwa kuwa fedha zipo, wakandarasi wanaendelea na kazi vizuri na usimamizi unafanyika kwa weledi, basi Watanzania wasiwe na shaka kwani mradi huo utakamilika na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.

”Lengo la kuanzisha mradi huu ni moja ya juhudi za Serikali za kupunguza gharama za umeme kwa wananchi kwa sababu uzalishaji wake ni wa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine. Uniti moja ya umeme unaozalishwa kwa kutumia maji inagharimu shilingi 36 hadi shilingi 50 huku umeme unaotumia vyanzo vya mafuta uniti moja inazalishwa kwa gharama ya shilingi 440 hadi shilingi 600.”

Aidha, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwahakikisha Watanzania kuwa serikali anayoiongoza itaendeleza miradi iliyoachwa na Hayati Dkt. John Magufuli kwa nguvu, kasi na ari ile ile aliyokuwa nayo.

Mradi huo ambao awali ulijulikana kwa jina la Stiegler’s Gorge unatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa Tanzania, nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi Afrika Masharika.