Majaliwa aingilia kati sakata la malori bandarini

0
216

Waziri Mkuu Kassm Majaliwa  ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ile ya Usimamìzi wa Bandari Tanzania (TPA) kushughulikia changamoto ya mifumo, ili kuondoa ucheleweshwaji wa utoaji mizigo katika bandari ya Dar es salaam.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Dar es salaam, wakati wa ziara yake ya kushtukiza bandarini hapo.

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika bandari ya Dar es salaam, inafuatia kuwepo kwa malalamiko yanayohusu ucheleweshwaji wa kutoa mizigo bandarini hapo.

Huko jijini Dodoma, Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania leo lililazimika kuahirisha mjadala wa bajeti wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa takribani dakika 20, kujadili sakata la malori kutoshusha wala kupakia mizigo kwa muda wa siku tano katika bandari ya Dar es salaam.

Hoja hiyo ya kuahirishwa kwa mjadala huo iliwasilishwa Bungeni na Mbunge wa Mafinga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Cosato Chumi.

Akiwasilisha hoja hiyo Chumi alisema kuwa bandari hiyo ndio chanzo kikubwa cha kuendeleza nchi na kufanikisha miradi, hivyo ni vema jambo hilo likashughulikiwa haraka.