Majaji watakiwa kuzingatia sheria

0
1087

Rais  John Magufuli amewaapisha Majaji wa Mahakama ya Rufani na wengine wa Mahakama Kuu aliowateua hivi karibuni na kusema kuwa kazi ya kusimamia haki ina changamoto kubwa, hivyo majaji hao wanatakiwa wamtangulize Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yao.

Wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam, Rais Magufuli pia ameshauri Majaji hao wapya kuzingatia sheria pamoja na katiba ya nchi katika utendaji kazi wao wa kila siku  hasa katika kuwahudumia Watanzania ambao  wengi wao wamekua walikosa haki yao ya kisheria.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ataendelea kuteua Majaji wengi zaidi  kadri bajeti itakavyoruhusu kwa kuwa bado mahitaji ya Majaji hao ni makubwa.

Kwa upande wa Wakuu wapya wa wilaya za Tarime mkoani Mara na Mwanga mkoani Kilimanjaro ambao nao amewateua hivi karibuni pamoja na Wakuu wengine wa wilaya nchini, Rais  Magufuli amewaagiza kutotumia madaraka yao vibaya na kuacha tabia ya  kuwaweka watu ndani pasipo kuzingatia utaratibu kama inavyofanywa hivi sasa na baadhi yao.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alipata fursa ya kuzungumza wakati wa hafla hiyo,  ambapo Majaji Sita wa Mahakama ya Rufani na wengine  Kumi na Watano wa Mahakama Kuu wameapishwa, huku wakuu wa wilaya mawili na Wakurugenzi Kumi wa halmashauri za wilaya wamepatiwa maelekezo ya kikazi na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma.

Akizungumza na watendaji hao, Makamu wa Rais ameelezea furaha yake kutokana na ongezeko la Majaji wanawake na kuwataka kufanya kazi huku wakiyatazama kwa ukaribu makundi mbalimbali ambayo yamekua yakilalamika kukosa haki.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa  Ibrahim Juma ametoa  wito kwa majaji hao  wapya  kufanya kazi kwa kujituma na kwa haraka ili kuweza kushughulikia mashauri mengi zaidi.

Ameelezea matumaini yake kuwa Majaji hao wapya watatenda haki na kutoruhusu malalamiko ya aina yoyote.

Majaji wa Mahakama ya Rufani walioapishwa katika hafla hiyo ni Sahel Barke, Jaji Mary Levira, Jaji Rehema Sameji,  Jaji Winnie Korosso, Jaji Ignus Kitusi na Jaji Lugano Mwandambo.

Majaji walioapishwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ni pamoja na Cyprian Mkeha, Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji Mwinshehe Kulita, Jaji  Ntemi Kilikamajenga,  Jaji Zepherine Galeba na Jaji Juliana Masabo.

Majaji wengine walioapishwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ni Mustapha Ismail,  Jaji Upendo Madeha,  Jaji Willbard Mashauri,  Jaji Yohane Masara,  Jaji Lilian Mongella,  Jaji Fahamu Mtulya,  Jaji John Kahyoza, Jaji Athumani  Kirati na Jaji Susan Mkapa.

Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya walioteuliwa ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi ni pamoja na Isaya Mbenje anayekwenda halmashauri ya  Pangani, Dkt Fatuma Mganga halmashauri ya  Bahi, Regina Bieda, -Tunduma, Jonas Mallosa halmashauri ya Ulanga, Ally Juma Ally anayekwenda Njombe  na  Misana Kwangura halmashauri ya Nkasi.

Wengine ni Diodes Rutema halmashauri ya Kibondo, Netho Ndilito halmashauri ya Mufindi, Elizabeth Gumbo halmashauri ya Itilima na Stephen Ndaki anayekwenda halmashauri ya Kishapu.

Wakuu wapya wa wilaya ni Charles Kabeho aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Tarime mkoani Mara na Thomas Apson ambaye anakua mkuu wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.