Majaji wapya kuchochea ufanisi wa mahakama

0
137

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amesema kuwa kabla ya majaji saba wa Mahakama ya Rufani hawajaapishwa leo kulikuwa na majaji 17 (akiwemo yeye), hivyo nyongeza hiyo inafanya jumla yao kuwa 24.

Aidha, kabla ya uapisho wa majaji 21 wa Mahakama Kuu wa Tanzania, kulikuwa na majaji 70, ambapo kati yao wanaofanya kazi za mahakama ni 64. Hivyo nyongeza hiyo inafanya majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (wanaofanya kazi za mahakama) wanafikia 85.

Akizungumza mara baada ya majaji hao kuapishwa ameeleza kuwa uteuzi huo utawezesha kurahisisha mhimili wa mahakama kutoa haki kwa wananchi na kupunguza idadi ya mashauri yanayosimamiwa na kila jaji.

Hata hivyo amewaonya kuwa majaji wana mamlaka kubwa sana, hivyo watumia mamlaka waliyopewa kuwatumikia wananchi, na kwamba hakuna aliyeomba nafasi hiyo bali wameaminiwa kuwa wanaweza.

“Rais amewapa imani kwamba ninyi ni watu safi mtatenda haki tupu, msipoteze hiyo imani,” amesema Prof. Juma.

Hafla ya uapisho imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo pia Makamau wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Spika Job Ndugai, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri mbalimbali.