Mahakama yapewa mamlaka kesi ya Sabaya

0
125

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imeipa mamlaka mahakama ya hakimu Mkazi Arusha kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake.
 
Ofisi ya DPP imewasilisha hati ya kuipa mamlaka mahakama hiyo leo kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
 
Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya Arusha, Patricia Kisinda Wakili Tarsila Gervas ameeleza kuwa DPP ametoa ridhaa kwa  mahakama hiyo ambayo ni chini kusikiliza kesi hiyo.
 
Amesema mahakama kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ila DPP chini ya kifungu cha 12(3) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ameona kwa maslahi mapana ya Taifa shauri hilo lisikilizwe katika mahakama hiyo ya chini.
 
Ole Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na utakatishaji fedha shilingi milioni 90.