Mahakama yaamuru Musiba kumlipa Membe Bilioni 6

0
168

Mahakama Kuu ya Tanzania, imemuamuru Mmiliki wa Gazeti la Tanzanite, Cyprian Musiba kumlipa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe kiasi cha Shilingi Bilioni 6 kama fidia ya kumchafua kupitia vyombo vyake vya habari.

Hukumu hiyo ya kesi namba 220 ya mwaka 2018 imetolewa na Jaji wa mahakama hiyo Joaquine De-Mello ambapo amesema mbali na mambo mengine Musiba anatakiwa kumlipa Membe Shilingi Bilioni 6.

Mahakama imesema Shilingi Bilioni tano ni fidia ya hasara halisi na Shilingi Bilioni 1 ni hasara ya jumla katika kesi hiyo ambayo Membe alimshtaki mahariri wa gazeti la Tanzanite Cyprian Musiba nakuwadai shilingi Bilioni 10 kwakumchafua.

Musiba katika kesi hiyo alishtakiwa kwa kumtuhumu Membe kuwa anamhujumu hayati Rais Dkt.John Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo huku akidai kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya ya kugombea urais mwaka uliopita.

Mahakama hiyo pia imetoa zuio la kudumu la Musiba kutomkashifu Membe au kusema uongo dhidi yake pamoja na kulipa gharama za zilizotumika kuendeshea kesi.