Magufuli: Majimbo katika nchi ni mwanzo wa mfarakano

0
405

Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amewataka Watanzania kufanya uchaguzi kwa makini na kuepukana na sera zinazotaka kuligawa Taifa kwa kuleta mfumo wa majimbo.

Akizungumza na wakazi wa Urambo mkoani Tabora ikiwa ni muendelezo wa kampeni za chama hicho amesema kuwa kuna baadhi ya vyama havina sera na kwamba vinataka kulirudisha taifa nyuma.

“…ukishatengeneza majimbo ya utawala katika nchi, huo ndiyo mwanzo wa mfarakano kwa sababu kila jimbo litakuwa linajitegemea lenyewe, likiwa masikini, litakuwa masikini wa kutupwa.”

Dkt. Magufuli amesema kuwa wakati wa kutafuta uhuru wa nchi, endapo Mwalimu Julius Nyerere angeigawa katika majimbo, Tanzania isingekuwa hapa ilipo leo.

“Tanzania tuna makabila zaidi ya 121, Nyerere alituweka sisi Watanzania kama taifa moja, ndio maana Tanzania tangu 1961 hatujaingia katika mfarakano wa kabila na kabila, kati ya dini na dini, kati ya maeneo na maeneo,” amesema mgombea huyo.

Dkt. Magufuli amesema endapo Tanzania itaingia katika machafuko, watu watatumia mwanya huo kujinufaisha wenyewe, hivyo ni lazima amani ilindwe.